UHUSIKA WA SAUTI KAMA MHUSIKA KATIKA UTEUZI NA UJENZI WA DHAMIRA KATIKA TAMTHILIA YA KISWAHILI: MFANO WA TAMTHILIA YA USINIUE (2019) YA ERIC F. NDUMBARO NA MARIA N. ISAYA
Furaha J. Masatu - PhD Candidate, The Open University of Tanzania, Tanzania
IKISIRI
Sauti ni miongoni mwa vitu ambavyo ni nadra kuviona vikitumika kama mhusika, aghalabu mhusika mtendaji mwenye nguvu kubwa ya ushawishi na adili kwa jamii kupitia kazi za fasihi andishi, hususani Tamthilia ya Kiswahili. Aina hii ya uhusika na mhusika ni maarufu zaidi katika kazi bunilizi za fasihi simulizi mathalani ngano, visasili na visakale. Kwa fasihi andishi, hasa tamthilia, kazi yenye mhusika Sauti ni pamoja na tamthilia ya Kivuli Kinaishi (1990) ya Said Ahmed Mohamed Khamis, ambayo mhusika Sauti anaonekana kuwa na nguvu kubwa ya ushawishi inayozaa mapinduzi dhidi ya utawala na uongozi dhalimu wa Bi. Kirembwe. Kwa mtalaa huo, makala haya yamechunguza namna mhusika Sauti (katika Tamthilia ya Usiniue) alivyoumbiwa nguvu na uwezo wa kutenda na kunena hata kuleta mabadiliko katika jamii kupitia uteuzi na ujenzi wa dhamira. Uchunguzi umeongozwa na nadharia ya Ontolojia ya Kiafrika ambayo pamoja na mambo mengine, inatambua nafasi ya sauti katika kuwakilisha Mungu, miungu, mapepo, majini na wahenga kwa njia ya matamko. Matamko hayo huweza kuwa ya kikorasi (kujirudiarudia kwa wazo au dhana kwa njia ya mwangwi au dhahiri) ama la. Kupitia uhusika wa mhusika Sauti, uchambuzi umebaini ya kwamba nguvu na ushawishi wa mhusika huyu ni mkubwa na umeibua dhamira tano (5) za msingi kabisa, ambazo ni: haki ya watoto kuishi na kulindwa, umuhimu wa utunzaji wa uumbaji wa Mungu, umuhimu wa kujiandaa sasa kwa faida ya maisha ya baada ya kifo, umuhimu na changamoto za sayansi na teknolojia ya habari na mawasiliano na umuhimu wa kufanya tathmini ya kina kabla ya kufanya uamuzi.